Tuesday, November 27, 2012

WAJUE MABILIONEA WATANO WATANZANIA

                                           WAFANYABIASHARA watano, Said Bakhressa , Dewji, Rostam Aziz, Reginald Mengi na Ali Mufuruki, wametajwa na Jarida la Ventures Africa linalozungumzia masuala mbalimbali ya uchumi wa Afrika kuwa ndiyo matajiri zaidi nchini.


Anayeongoza katika orodha hiyo ni Bakhressa anayemiliki mali na fedha zenye thamani ya Dola za Marekani 620 milioni sawa na Sh992 bilioni (Dola moja Sh1,600) akifuatiwa na Dewji ambaye utajiri wake ni Dola 560 milioni (Sh896 bilioni). Wengine na kiasi cha mali na fedha wanazomiliki kwenye mabano ni Rostam (Sh672 bilioni- Dola 420 milioni) Mengi (Sh448bilioni- Dola 280 milioni) na Mufuruki (Sh176 bilioni - Dola 110 milioni).

Matajiri hao wamepatikana baada ya kuangalia nafasi zao kifedha, ufanisi wa kampuni zao katika soko la hisa, mfumo wa wanahisa katika soko la hisa na mtiririko mzima wa fedha katika akaunti zao kwenye benki mbalimbali.

Jarida hilo linalotoka mara moja kwa mwezi kutoka Afrika Magharibi, limesema matajiri hao wa Tanzania ni kati ya Waafrika wenye utajiri ambao ni mabilionea 4,800 kutoka mataifa 17.
Asilimia kubwa ya watu 1,523 ni mamilionea na wamo katika ripoti ya watu matajiri Afrika.
Jarida hilo linataja jinsi matajiri hao walivyokuwa wajasiriamali wadogo kabla ya kuibuka na kuwa mabilionea.
                                                                                                                                                                 
Said Salim Bakhresa 
          Jarida hilo limesema chanzo cha utajiri wa Bakhressa ni mapato yanayotokanana uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kwenye viwanda vyake.

Mfanyabiashara huyo aliacha shule akiwa na umri wa miaka 14 na kuanzisha biashara zake. Alianza kuuza urojo Zanzibar na baadaye alifungua mgahawa miaka ya 1970.

Mgahawa huo ulipanuka na alitumia faida yake kufungua mashine ya kusaga pamoja kiwanda za usindikaji vyakula, huku akiunda Kundi la Makampuni ya Bakhressa.
Aliendelea kusindika vyakula mbalimbali na kutengeneza unga wa mahindi na baadaye kuanzisha kiwanda cha kuoka mikate na baadaye kutengeneza chocolate, ice cream, vinywaji na makasha ya kufungashia bidhaa. Kutokana na shughuli hizo, kwa mwaka huingiza Sh800 milioni.
Kampuni zake kwa sasa zinafanya biashara mbalimbail katika nchi za Tanzania, Uganda, Malawi, Rwanda na Msumbiji na ameajiri zaidi ya wafanyakazi 2,000.


                                      
Gulam Dewji 
        Mfanyabiashara huyo ana utajiri unaokadiriwa kufikia Dola 560 milioni kutokana na kuzalisha bidhaa na kutoa huduma mbalimbali.
Ni mmoja wa mataikuni wa Tanzania tangu miaka ya 1970 na kazi yake kubwa ilikuwa kuingiza bidhaa mbalimbali kutoka nje.

Alianza na kampuni ndogo aliyoiita Mohammed Enterprises Tanzania, ambayo kwa sasa ni kati ya kampuni kubwa Afrika Mashariki na Kati.
Miongoni mwa mali zake ni Kiwanda cha 21st Century Textiles, moja ya viwanda vikubwa vya nguo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Kampuni yake ina viwanda vinne, Tanzania na Msumbiji huku ikizalisha Dola 100 milioni kwa mwaka. Pia kampuni hiyo husindika juisi kwa matunda ya Tanzania, mafuta ya kula, sabuni na tishu.

Kampuni hiyo pia inamiliki kampuni ya bima, makontena, kampuni za kuuza mafuta ya petroli na maduka ya kuuza bidhaa mbalimbali zaidi ya 100 Tanzania nzima.
Hata hivyo, Gulam alisema jana kwamba takwimu zilizotolewa zimekosewa. Alisema kwa sasa yuko nje ya Dar es Salaam na atatoa taarifa sahihi atakaporejea.
“Kuna baadhi ya tarakimu zimekosewa niko Morogoro kuangalia biashara zangu nikirudi Dar es Salaam nitazungumza,” alisema Dewji.
                                      
Rostam Aziz
              Ameelezwa kuwa utajiri wake umetokana na kuendesha shughuli zake mbalimbali ikiwamo kampuni za mawasiliano ya simu, madini na biashara za usafiri wa meli.
Mwanasiasa huyo mwenye asili ya Asia, alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mbunge wa Igunga mwaka 1993 na alishinda kwa vipindi viwili.

Aliachana na ulingo wa siasa mwaka 2011. Anamiliki asilimia 19 ya Hisa za Kampuni ya Vodacom ambayo ina wateja zaidi ya milioni nane.

Ameelezwa pia kuwa anamiliki Kampuni ya Ujenzi ya Caspian na sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Kampuni ya Hutchison Whampoa ya Hong Kong.
Akizungumzia utafiti huo, alisema: “Umefanyika kwa umakini isipokuwa tu kwa upande wangu wanasemas ninamiliki asilimia 19 ya Kampuni ya Vodacom kitu ambacho si sawa kwani ninamiliki asilimia 35.”                     
Reginald Mengi
              Mengi anakimiliki kampuni mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari, viwanda vinavyozalisha vinywaji baridi vya Coca-Cola na ana mgodi wa dhahabu.
Mfanyabiashara huyo baada ya kufanya kazi ya uhasibu ambayo ndiyo taaluma yake, alifanya biashara ya kutengeneza kalamu za wino zilizopata soko kubwa Afrika Mashariki.
Leo hii, IPP Group ambayo Mengi ni mwenyekiti wake, inamiliki magazeti mbalimbali ikiwemo Financial Times, ThisDay na The Guardian, televisheni mbili kubwa Afrika Mashariki na Kati EATV na ITV na vituo vya redio. Anamiliki Kampuni za IPP Gold na Handeni Gold.
                             
Ali Mufuruki
               Utajiri wake unatokana na biashara mbalimbali za rejareja na za ushirika.
Ni mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa Tanzania Infotech Investment Group.
Kampuni hiyo inajumuisha Watanzania na Waganda kwa ajili ya kuuza bidhaa za Afrika Kusini za Woolworth.Infotech hufanya kazi ya uendelezaji makazi na ukodishaji, matangazo na shughuli za mawasiliano.
           

No comments:

Post a Comment