Wednesday, August 22, 2012

UFAHAMU UGONJWA WA EBOLA

Mgonjwa wa Ebola akipata huduma

Ebola ni ugonjwa wa hatari unaosababishwa na virusi vijulikanavyo kwa lugha ya kitaalamu Ebola Virus .
Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kitaalamu kama  ‘homa za virusi’ na husambazwa na damu kutoka kwa mtu mwenye virusi hivyo kwenda kwa ambaye hana ugonjwa baada ya kutokwa na damu yule aliyeathirika.
 Kwa kitaalamu hali hiyo ya maambuziki huitwa Viral Haemorrhagic Fevers na chanzo kamili cha virusi vya ugonjwa huu hakijulikani kama ilivyo hali inayosababisha mlipuko wake pia haijulikani. Maradhi haya hayana tiba  tiba wala chanjo.
DALILI
Dalili za ugonjwa huu zipo nyingi lakini muhimu ni hizi, kwamba mgonjwa anakuwa na  homa kali, inayoambatana na kutokwa damu katika matundu yote ya mwili kama vile puani, njia ya haja kubwa na ndogo, masikioni, mdomoni, machoni  au anaweza kupasuka ngozi n.k.
Dalili nyingine ni kutapika damu, kuharisha damu,  fizi kuvuja damu, kutokwa na damu na kuvia chini ya ngozi au kutokwa na damu sehemu za haja kubwa na ndogo, choo na mkojo pia vitaonekana kuwa na damu. Ugonjwa huu  huweza kuenea kwa jamii kirahisi na haraka  sana kutoka mtu mmoja hadi mtu mwingine kupitia njia mbalimbali kama vile kugusana, kwa njia ya mate, damu, mkojo, machozi, kamasi au kwa njia ya majimaji mengine ya mwili,ikiwa ni pamoja na jasho. Mtu anaweza kupatwa maambukizi kwa kumgusa  mtu aliyekufa kwa ugojnwa wa Ebola au kuchomwa sindano ambayo mwenye maradhi haya amechomwa nayo na vile vile huambukiza kwa njia ya kujamiiana.
Lakini  vifaa ambavyo ametumia mtu mwenye maradhi haya vikitumiwa , mtumiaji anaweza kupatwa na ugonjwa huu.
KINGA
Ugonjwa wa Ebola unaweza kuzuilika kwa kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, machozi na majimaji mengine yanayotoka katika mwili wa aliyeathirika au mtu mwenye dalili za ugonjwa huu wa Ebola.
Ili kujikinga ni vema wananchi wakatoa taarifa mapema kwa viongozi hasa wa afya mara tu waonapo mtu mwenye dalili za ugonjwa huu. Wakati huo huo ni vyema kumuwahisha hospitali mgonjwa mwenye dalili tulizozitaja hapo juu.
Wananchi waepuke kuishughulikia maiti ya mtu aliyefariki kwa ugonjwa au dalili za ugonjwa wa Ebola na badala yake waiarifu serikali ambayo itatoa wataalamu wenye vifaa maalum wa kuzika na kuipima maiti ili kujua kama aliambukizwa maradhi hayo au la.

No comments:

Post a Comment