Wednesday, August 29, 2012

MATESO YA VENGU, CHANZO NI ORIJINO KOMEDI WENYEWE


Joseph Shamba 'Vengu'.
TABIA za wasanii wa Kundi la Orijino Komedi ni tatizo kubwa. Unaweza kujiuliza kwa nini sasa hivi wasanii hao wamepoteza mvuto kwenye jamii. Mtindo wa maisha yao hauna mvuto.
Endapo mtindo wa maisha yako utakuwa unawafurahisha watu, utaendelea kupendwa. Ikitokea unawaudhi watu, mvuto wako lazima utapotea. Komedi wajiangalie leo, kwa nini hawana mvuto?
Wajipime walivyokuwa mwaka 2007 hadi mwaka 2009, waone namna walivyoishika nchi. Baada ya hapo wajiangalie walivyogeuka wa kawaida kuanzia mwaka 2009 mpaka sasa.
Huwezi kuwakera watu halafu wakaendelea kukupenda. Asili yetu Watanzania ni kuwakumbatia watu wema. Inawezekanaje watu wabaguzi, wanaowanyanyapaa wengine, wakakubalika kwenye jamii yetu?
Ni jambo lisilowezekana. Ndiyo maana Orijino Komedi leo hii hawana mvuto. Dhambi ya kumbagua Vengu (Joseph Shamba), kumfanya aishi kama mtwana wao wakati ni mwenzao, haiwezi kuwaacha salama.
Dhambi ya kuwadhihaki watu ambao uchumi wao siyo mzuri, wakiwasema eti wamefulia, wakati nao bado ni wasafiri kwenye haya maisha, haiwezi kuwaacha salama. Kuna matokeo lazima yawakute.
Ni lazima walipe gharama za vitendo vyao viovu. Gharama hizo ndiyo matokeo ya sasa tunayoyaona. Namba ya watazamaji wa vipindi vya Orijino Komedi, imeshuka kwa kiasi kikubwa mno.
Siyo siri, kipindi cha nyuma Komedi ilikuwa ndiyo habari ya mjini. Kila Alhamisi jioni ilikuwa ni hekaheka kwenye runinga. Baa zilifurika, vibanda vya video show (vibanda umiza) vilijaa kupita kiasi. Waliteka jamii kisawasawa.
Kuna wakati Komedi ilirejesha amani ya nyumba, kwani baba na mama, walijumuika pamoja na watoto kila Alhamisi jioni, sebuleni kutazama vichekesho vya vijana hao.
Watu hao wamewakimbia. Ni matokeo ya tabia ambazo si njema walizozionesha. Ni malipo yao baada ya kubweteka kwa kudhani wameshafika kwenye kilele cha maisha. Hadhi yao imeshuka mno.
Zamani Komedi ilikuwa programu inayowalazimisha watu kutenga muda wa kutazama vichekesho vyao. Hivi sasa, wenye kiu ya kutazama ni watoto na kwa watu wazima, ni wale waliokuta runinga imewekwa TBC1, wakaona wapoteze muda huku wakijiuliza: “Hivi hawa kumbe bado wapo?”
Kama msemo wao wenyewe, ni wazi Orijino Komedi wamefulia. Hata idadi ya matangazo waliyokuwa wanapata zamani hivi sasa hawana. Hii iwape sababu ya kujipima, waangalie makosa yao, la sivyo watapotea kabisa.
Ni vijana wenye vipaji, kwa hiyo ni vizuri wakatetea ajira zao. Wabadilike leo. Waache kubweteka, wao bado ni wachanga mno. Maisha ni safari ndefu, naamini wakijirudi, jamii itawapenda tena.
Hivi hawajiulizi leo Ze Comedy ya akina Bambo (Dickson Makwaya), inavyoteka soko la vichekesho nchini kupitia Channel 5 (EATV)? Unapoona akina Mtanga wanageuka habari ya mjini, maana yake Joti na Mpoki, kwisha habari yao.
Kushuka kwa akina Joti, inawezekana ikawa ni matokeo pia ya jeuri yao waliyomuonesha mzee Reginald Mengi wakati ndiye aliyewafanya wakaonekana hapa nchini.
Nawashauri wajirudi, watubu mateso waliyomsababishia Vengu mpaka wakamfanya awe chapombe. Mbaya zaidi, hata walipoambiwa kwamba msanii huyo ana hali mbaya, wapo waliojibu, “atajijua.”
Kijana wa watu anateseka, amenyang’anywa gari, ikadaiwa hata fedha zake nyingi zimefichwa kwenye akaunti ya mmoja wa wasanii wa kundi hilo (jina ninalo na habari hiyo iliandikwa gazetini). Mateso hayo ya moyo, yakamfanya ajiliwaze kwa pombe.
Huko kwenye pombe, akawa anazitwika mpaka anakuwa ‘tilalila’. Anapoteza fahamu, sisi Global Publishers, tunawapigia simu wasanii wenzake, wajitokeze kumpa msaada, msanii mmoja (jina ninalo), akajibu: “Huyo atajijua yeye mwenyewe.”
Ni mateso yaliyoje kuishi kwenye jamii ya watu ambao hawakupendi? Hayo ndiyo maumivu makubwa aliyoishi nayo Vengu. Hii ikamfanya awe rafiki mkubwa wa pombe ili ajiliwaze kwa machungu ya kubaguliwa na wenzake.
Kwa hakika, jumlisha mateso ya kubaguliwa na wenzake, jumlisha na maradhi yaliyomchukua kwa muda sasa, ni wazi msanii huyo hajawahi kufurahia maisha ya kundi hilo kama ilivyo kwa wenzake.

No comments:

Post a Comment