Tarehe 23/05/2012 leotainment.blogspot.com iliandika makala inayosema: ‘Ay na B’Hits na urafiki uliochuja kimya kimya’. Makala hiyo ilijaribu kuangalia uhusiano wa Ambwene Yesaya na Hermy B ambaye ni producer na mwenyekiti mtendaji katika kampuni ya B’Hits Music Group.
Hermy B ambaye ameisoma makala hiyo, ameandika email kukanusha baadhi ya mambo waliyoyaandika na pia kutoa ufafanuzi wa namna mambo yalivyokuwa na yalivyo sasa:
"Ningependa kujibu shutuma zilizoandikwa na blog yako kuhusu uhusiano wangu na swahiba wangu A.Y. Ningependa ifahamike kwamba mimi na A.Y kwa kipindi cha miaka 4 tumefanya kazi za muziki kwa karibu pamoja na kazi nyingine za biashara. Ni kawaida na inaeleweka kwamba mahali popote watu wanapofanya kazi pamoja kugongana katika mawazo au lugha ni jambo la kawaida, na ndio changamoto zenyewe. Si jambo la ajabu kama mimi na swahiba wangu A.Y. kupishana katika kazi.
Baada ya kusoma makala inayonihusu kwenye blog yako nimeona ni umuhimu wa kujibu ni makala yako haswa kuhusu swali linalohusu utu na tamaa ya pesa. Kwanza ningependa ieleweke kwamba umeniweka katika picha ya mtu mwenye tamaa kubwa ya pesa na nisiejali utu picha amabayo imeanza kunisumbua katika shuhuli zangu kwa muda mfupi tu kwani wananchi wameanza kuniona hivyo.
Hivyo nimeona ni lazima nijibu kwani nikiiacha bila kujibu madhara yake yatakuwa mabaya. Kwanza napenda uelewe sijawahi kuwa msimamizi wa kazi za A.Y zaidi ya kuwa producer wa nyimbo zake tu. Kipindi chote hicho nimekua natumia utaalamu wangu kwenye kutengeneza tu muziki wake. Maswala mengine yoooote amekuwa akifanya mwenyewe tena bila msaidizi.
Pia ufahamu bila A.Y na MwanaFA kunipa nafasi kutengeneza muziki wao nisingekua hapa nilipo. Nadhani inaeleweka mahali popote duniani kwamba kipaji ili kifahamike kwa watu lazima kipitie kwa mtu fulani au mkondo fulani. Si ajabu kama kipaji changu cha kuproduce muziki kimeweza kufahamika kwa kupitia kwa A.Y. Mimi sio mungu labda ningekua sehemu nyingine na mafanikio makubwa zaidi au machache zaidi,lakini nachojua rafiki yangu amenipa ngazi ya kufika huku nilipo sasa, sijawahi kuficha hilo na hata wao wenyewe wanajua na bado nashukuru kwa hilo.
A.Y hajawahi kuingia mkataba wa aina yoyote na kampuni ya BHits Music Group Limited wala mimi binafsi uliombana kufanya kazi na mimi na sio mtu mwingine yoyote. Nimetengeneza nyimbo zisizopungua 30 za A.Y, kwa ajili ya albamu yake katika kipindi cha mwaka 2008 mpaka 2011. Baadhi ya nyimbo hizo zimeshatoka na nyingine bado zipo zikisubiri uhitaji wake. Wote tulikua na lengo la kutengeneza muziki kwa wingi na kuuza kwenye soko zuri la muziki ili tufaidike kwa pamoja.
Muda wote muziki ulikua unatolewa na unafanya vizuri kwa radio na T.V na show zilikua zinafanyika na zote nilikua nazijua iwe ndani ya nchi au nje ya nchi hii hata malipo nilikua nafahamu ni kiasi gani na sijawahi kufichwa na A.Y kuhusu hilo.
Utata umekuja kwenye malipo yaliyotajwa kwenye blog yako ambayo yameniudhi sana na baadhi ya wasanii wanaopenda kurekodi kwangu wameanza kuwasiliana na mimi kuuliza bei imepanda lini na kama inawahusu pia.
Kutoelewana kwetu kwetu kibiashara ilikuwa mwezi February mwaka huu yakihusu malipo ya album hiyo. Baada ya hapo niliamua kufunga mdomo wangu na nisingesema chochote kwani haya yalikua yananihusu mimi na rafiki yangu tu. Nimeamua kuongea sasa kwani nahisi nimeshambuliwa kwa mara ya pili kuhusu makubaliano haya na mara ya kwanza niliamua kukaa kimya.
Kwanza nataka ufahamu Katika kipindi cha kutokea 2008 mpaka leo hii (miaka 4) kwa matumizi ya nyimbo hizo, ambazo amekwishafanyia show nje na ndani ya nchi na nyingine kumpatia nominations na tuzo tofauti, nilichowahi kulipwa hakitaweza kuzidi shilingi milioni tatu kwa malipo ya awamu tofauti kwa miaka minne.
Kilichotokea ni kwamba, mwaka huu mwanzoni kabisa, A.Y aliwasiliana na mimi akiwa na mipango ya kuzindua albamu yake. Na alitaka kuzinunua zile nyimbo kutoka kwangu akiwa na mpango mpya wa kuiuza albamu kwa mpango wake binafsi pasi na mimi. Nilishindwa kuelewa nini anakifanya hasa alipoomba alipie wimbo mmoja mmoja tena kwa bei ya msanii wa kawaida anaehangaika kutoka.
Niliamua kukubali kwamba ameamua kufanya hivyo na sina nguvu ya kumzuia basi nikajaribu kupata malipo halisi ya kazi yangu. Ubishi wangu ulikua kwamba msanii mdogo hawezi kulipa bei sawa ya kurekodi na msanii mkubwa, kwani hata malipo ya msanii mkubwa na mdogo baada ya kazi yoyote iwe ya matangazo ama show huwa hayafanani. Bei niliyotaja haikua millioni kumi, ni uongo mtupu na kwa wimbo mmoja niliomba nilipwe millioni 2.
Akakubali kwa bei hiyo ya Millioni 2 japo nilihisi hakuridhika kabisa. Nilimtumia mkataba wa makubaliano yetu ambayo kweli baadae aliona kwamba bei hiyo kwake ni kubwa sana hivyo hatukusaini makubaliano. Tulibadilishana meseji kwa simu kwa muda mrefu sana na niliona biashara hii itavunja urafiki wetu.
Nilifikiria sana kwamba nyimbo hizi nimekaa nazo toka 2008 bila kuingiza chochote na maisha yanaenda pia. Sikuona sababu ya kuharibu urafiki wetu wa muda mrefu kwa mabishano haya. Kwa Ujumbe wa simu nilimueleza A.Y anakaribishwa aje achukue nyimbo zoooooote anazohitaji kwa albamu yake BURE (bila malipo).Lakini nilimuomba anisamehe sitomix zile ambazo bado hazijamixiwa, ila ampatie producer mwingine amfanyie hiyo kazi.
Mpaka naona hii makala A.Y hajaja kuchukua hizo nyimbo na ndio naelewa kua hayupo na BHits tena na wala taarifa zote hizo mbili hajawahi kunipatia. Huu ndio ukweli halisi.
Swala la mimi kuwa na wivu na kinyongo na mafanikio ya A.Y ni uongo na nashangaa umetoa wapi maneno hayo. Kama kulipwa kidogo, huku nikiona A.Y anaingiza fedha nyingi kwa muziki tunaotengeneza pamoja basi ningekua nimegombana nae toka mwaka 2009 labda.
Narudia kwamba nilikua najua kila show yake inapofanywa na sikuwahi kujisikia vibaya. Nataka utambue pia nilikua na akili timamu wakati nafanya kazi na A.Y na muda wowote nilikua na uwezo wa kubadili mawazo na kutaka tuandike makubaliano kwa karatasi ila sikufanya hivyo na wala sijutii chochote kwa utaratibu wetu wa hatari wa kufanya kazi bila mkataba wa maandishi na ndio maana nipo radhi hata sasa kumpatia nyimbo hizo bure kama nilivomwambia hapo mwanzo.
No comments:
Post a Comment