Sofia Rashid (22) mkazi wa Chanika
jijini Dar es Salaam yupo njia panda kwa kutojua hatma ya watoto wake
wawili ambao wote wamekumbwa na maradhi ya ajabu ya kujaa maji kichwani.
Watoto hao Omar Mohamed (4) na Maulidi
Mohamedi mwenye umri wa miezi minne wamelazwa katika Taasisi ya Tiba ya
Mifupa Muhimbili (MOI) kwa ajili ya kupatiwa tiba.
Akiongea akiwa wodini, Sofia alisema
anakabiliwa na mateso moyoni mwake pale anapowaona watoto wake
wanavyoteseka kwa maradhi hayo.
Alisema watoto wake wote walizaliwa
wakiwa na maradhi hayo ambapo walipofikia miezi miwili walianza na
tatizo la kichwa kukua kwa haraka na kusababisha ashindwe kuwabeba.
Sofia alisema kwamba kutokana na
matatizo ya watoto wake, mume wake aliyemtaja kwa jina moja la Mohamed
alimpa talaka kwa madai hawezi kuishi naye kwa sababu anazaa watoto wa
ajabu.
Alieleza toka apewe talaka baba wa watoto hao hajakwenda kumjulia hali wala kumpatia huduma muhimu kwa ajili ya watoto hao.
“Inaniuma sana nikiona hali hii, mimi
sikupenda kuzaa watoto hawa ila Mungu amepanga, lakini mwenzangu
ananiona kama mimi ndiye mwenye tatizo na kuamua kuniacha,” alisema.
Endapo ukifika kwa mara ya kwanza na
kuwaona watoto hao wakiwa wamelala kwenye kitanda kimoja wodini hapo,
hautaweza kugundua kwa haraka umri wao kama hautaelekezwa na mama yao
ambaye muda wote anakaa karibu nao kwa ajili ya kuwapatia msaada.
“Hawa hawajazaliwa wakati mmoja, huyu
Omar ana miaka minne na mdogo wake ana miezi minne tu, lakini kutokana
na ugonjwa hauwezi kumtambua nani ni mkubwa kiumri,” alisema mama yao
baada ya kuulizwa umri wao na mwandishi wa gazeti hili.
Hata hivyo, alisema licha ya kupatiwa
huduma mbalimbali za matibabu kwenye hospitali hiyo, bado anapambana na
matatizo mbalimbali ikiwemo kukosa pesa ya kununulia chakula pamoja na
mavazi ya watoto hao pamoja na yeye mwenyewe.
“Hapa nilipo sina nguo wala chakula kwa
ajili ya watoto na mimi mwenyewe, namshukuru dada yangu kwa kunipa
msaada lakini kutokana na kutokuwa na kazi maalum inakuwa vigumu
kunitosheleza mahitaji,” alisema.
Sofia aliwaomba wasamaria wema
watakaoguswa na matatizo yake kumsaidia kwa hali na mali kwa ajili ya
kumsaidia kumpatia pesa za kujikimu akiwa wodini hapo.
Afisa Uhusiano wa MOI, Almas Jumaa
alisema Sofia na wanawe walifikishwa hapo miezi minne iliyopita, ambapo
madaktari wanajitahidi kutoa huduma za kuokoa maisha ya watoto hao
ikiwemo kuwafanyia upasuaji wa kichwa.
Alisema baada ya kuwafanyia uchunguzi
imebainika watoto hao wanasumbuliwa na matatizo ya kichwa kujaa maji na
tiba yake inafanyika hospitalini hapo.
Kwa yeyote anayetaka kumsaidia Sofia kwa
huduma ya chakula, mavazi awasiliane na Afisa Uhusiano wa Moi Almas au
afike ofisi ya gazeti hili Mikocheni na kuwasiliana na Moshi Lusonzo kwa
namba 0717 336368.... nipashe jumapili...
No comments:
Post a Comment