HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO
KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA,
KWA WANANCHI, TAREHE 31 JULAI, 2012
Ndugu
Wananchi;
Naomba nianze kwa kuomba radhi kwa kutoa hotuba ya mwisho wa
mwezi wa saba, leo tarehe 01 Agosti, 2012 badala ya jana tarehe 31 Julai,
2012. Hii ni kwa sababu ya msiba
uliotukuta katika familia na mimi kwenda Lindi kushiriki maziko ya marehemu
wetu. Tofauti na miezi iliyopita leo,
pamoja na hotuba ya kawaida ya mwisho wa mwezi nimetoa fursa kwa Wahariri wa
vyombo vya habari nchini kuniuliza maswali nami kujibu. Kwa upande wangu nina mambo matatu ambayo nitayazungumzia leo.
Ajali ya Kuzama kwa Meli ya MV SKAGIT
Ndugu Wananchi;
Jambo la
kwanza ni ajali ya Meli ya MV SKAGIT iliyotokea tarehe 18 Julai, 2012. Meli hiyo ilikuwa na watu 290, wakiwemo mabaharia 9, abiria watu wazima 250 na watoto 31. Juhudi za uokoaji
zilianza mara baada ya taarifa ya kuzama kwa meli hiyo kupatikana. Maofisa na askari wa JWTZ, Polisi na KMKM
walishiriki pamoja na meli na watu binafsi katika uokoaji. Waokoaji walifanikiwa kuwapata ndugu zetu 146 wakiwa hai na maiti 126 hadi tarehe 27 Julai, 2012. Kwa maana hiyo basi, watu 18 hawajulikani
walipo na inahofiwa kuwa nao pia hawako hai.
Huenda wamezama pamoja na meli au walizama baharini lakini miili yao
haikuweza kupatikana.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kurudia kutoa mkono wa rambirambi na pole nyingi kwa wale
wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali ile. Nampongeza sana Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na
viongozi wenzake wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kazi kubwa na
nzuri waliofanya kuongoza juhudi za uokoaji pamoja na huduma walizotoa kwa waliokolewa,
waliojeruhiwa na waliofariki. Kwa wale
ambao walikuwa wenyeji wa Unguja na Pemba, SMZ ilitoa sanda na usafirishaji wa
maiti mpaka makwao kwa mazishi. Kwa wale
wasiokuwa na ndugu Serikali ilibeba jukumu la kuwazika kule Kama, Kusini
Unguja.
Natoa pongezi
za pekee kwa wale wote walioshiriki katika uokoaji kwani juhudi zao ziliwezesha
ndugu zetu wengi kusalimika na maiti nyingi kupatikana.
Ndugu Wananchi;
Kutokea kwa ajali
ile kumetonesha jeraha la huzuni, majonzi na mashaka makubwa yaliyolipata taifa
letu miezi 11 iliyopita kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya MV Spice
Islander. Katika mkutano maalum wa
Baraza la Usalama wa Taifa niliouitisha tarehe 20 Julai, 2012 kuzungumzia ajali
ya MV SKAGIT tulifanya mapitio ya utekelezaji wa maagizo yetu ya mkutano wa
tarehe 11 Septemba, 2011 kufuatia ajali ya MV Spice Islander. Kwa ujumla tumeridhika kuwa utekelezaji
umekuwa mzuri kwa upande wa mamlaka zinazohusika na usafirishaji majini yaani SUMATRA,
Zanzibar Maritime Authority na mamlaka za Bandari za nchi zetu mbili. Ushirikiano baina ya mamlaka hizo sasa ni
mzuri kwa mambo yote muhimu ambayo Baraza liliagiza wafanye hivyo. Pamoja na hayo Baraza limetaka ushirikiano
huo uzidishwe na kuimarishwa.
Kwa mfano, Baraza
limefurahishwa na kupongeza kitendo cha
mamlaka hizo kutumia Dar es Salaam Maritime Institute kwa ushauri kuhusu ubora
wa meli na huduma za usafirishaji majini.
Baraza limeagiza vyombo hivyo viwe
na hadidu za rejea zinazofanana kwa vigezo vya ubora ili nchi yetu iwe na viwango vinavyofanana vya ubora wa meli na
huduma za usafirishaji baharini kwa pande zetu mbili za Muungano. Bahari ni moja na vyombo vinahudumia watu
wale wale, kuwa na vigezo tofauti vya ubora wa meli na viwango vya huduma ni
jambo lisilostahili kuwepo tena, ni la hatari.
Baraza pia limeagiza pawepo na ukomo wa umri wa meli zilizokwishatumika
zinazoruhusiwa kutumika hapa nchini.
Aidha, Baraza
limerudia kuagiza pawepo na usimamizi makini zaidi kuhusu upakiaji wa mizigo na
abiria. Mamlaka husika, yaani SUMATRA,
ZMA na maofisa wa bandari wahakikishe
kuwa uwezo wa meli uliohakikiwa na kutambuliwa unaheshimiwa ipasavyo. Pia, meli zikaguliwe mara kwa mara na vigezo
vifanane.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na
hayo, Baraza la Usalama wa Taifa limeona kuwa wakati umefika kwa Serikali yetu
kuwa na Coast Guards, yaani kikosi maalum cha uokoaji na usalama majini. Aidha, Baraza limetaka hatua za makusudi zichukuliwe
kuimarisha KMKM na Police Marines.
Mwisho, Baraza lilipongeza uamuzi wa SMZ wa kuunda Tume ya kuchunguza
ajali ile kama ilivyofanya wakati wa ajali ya MV Spice Islander.
Utafutaji
na Uchimbaji Gesi Nchini
Ndugu
Wananchi,
Jambo la pili
ninalopenda kulizungumzia leo ni kuhusu maendeleo ya sekta ya gesi asili
nchini. Juhudi za kutafuta mafuta nchini
zilianza mwaka 1952 na mwaka 1954 wakati kampuni ya BP ilichimba kisima cha kwanza
kule Mafia. Bahati mbaya kisima hicho
hakikuzaa matunda yaliyotarajiwa na juhudi za utafutaji mafuta zikafifia kabisa
mwanzoni mwa miaka ya 1960. Miaka kumi
baadae, juhudi hizo zilianza upya na kuendelea kwa kiwango na kasi za namna mbalimbali
hadi sasa. Katika miaka ya hivi karibuni
juhudi zimekuwa kubwa na kuhusisha makampuni kadhaa ya kimataifa yakiwemo
makubwa na madogo.
Ndugu Wananchi;
Tangu mwaka
1954, mpaka sasa visima 61 vimechimbwa,
kati ya hivyo, gesi asili imegunduliwa katika visima 22, visima 14 vya nchi
kavu na maeneo ya maji mafupi na visima 8
vya bahari ya kina kirefu. Hatujabahatika
kupata mafuta lakini tumefanikiwa kupata gesi asili katika maeneo kadhaa
baharini na nchi kavu katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.
Kwa mujibu wa
taarifa zilizopo kutokana na visima vilivyochimbwa mpaka sasa, akiba ya gesi
asili iliyopo nchini inakadiriwa kuwa kati ya futi za ujazo trilioni 25.4 – 28.9. Yapo matumaini makubwa ya gesi nyingi zaidi
kugundulika katika miaka michache ijayo.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba shughuli za utafutaji mafuta na hasa gesi
baharini zilizoanza mwaka 2004 kukiwa na kampuni moja sasa zipo 18. Baada ya ugunduzi wa kwanza wa gesi
mwaka 2010, shughuli za utafutaji sasa zimepamba moto na zimekuwa na
mafanikio. Naamini gesi nyingi zaidi itaendelea
kupatikana.
Fursa za Maendeleo
Ndugu Wananchi;
Kwa
kiasi cha gesi asili kilichokwishagunduliwa na kwa matumaini yaliyopo ya gesi
zaidi kupatikana kunaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi za kutumainiwa duniani
kwa upatikanaji wa gesi asili miaka michache ijayo. Hali hiyo inaipa nchi yetu fursa kubwa ya
kuweza kujiletea maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii muda si mrefu kutoka
sasa.
Gesi
asili ni rasilimali inayoweza kutumika kuzalisha mbolea na hivyo kusaidia
katika kuendeleza kilimo nchini kwa kurahisisha upatikanaji wake na kuwa ya bei
nafuu. Gesi asili inaweza kutumika
kuzalisha umeme na hivyo kuiwezesha nchi kupata umeme wa kutosha na kuwepo
ziada ya kuuza nje. Hivi sasa, katika
gridi ya taifa megawati 350 za umeme
zinatokana na gesi asili na hata lengo letu la kuzalisha megawati 3,500 ifikapo maka 2015 tunategemea zaidi gesi asili
kuwezesha hilo kutimia. Ujenzi wa bomba
la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam una shabaha hiyo.
Ndugu Wananchi;
Vile
vile, gesi asili inaweza kutumika kutoa nishati viwandani badala ya kutumia
mafuta na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji. Watu majumbani wanaweza kutumia gesi asili
kupikia hivyo kupunguza matumizi ya umeme, mafuta, mkaa na kuni. Inapunguza gharama za maisha na kusaidia
kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti. Ni kutokana na kutambua ukweli huo ndiyo
maana TPDC inatekeleza mradi wa kutengeneza gridi ya mabomba ya kusambaza gesi
majumbani katika jiji la Dar es Salaam.
Jambo
lingine muhimu kuhusu rasilimali hii ni kwamba tukiuza nje gesi nchi yetu itapata
mapato mengi tena ya fedha za kigeni.
Kwa vile gesi ni nyingi mapato ya Serikali yataongezeka sana, hivyo
kuijengea uwezo wa kutimiza majukumu yake vizuri zaidi. Kama matumizi yatakuwa mazuri, gesi asili itakuwa
kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi wa nchi.
Maendeleo ya haraka yatapatikana na hivyo kusaidia kuwaondoa wananchi
wengi kutoka katika lindi la umaskini tulionao sasa.
Changamoto
Muhimu
Ndugu Wananchi;
Pamoja na
ukweli kwamba kuwa na gesi asili nyingi kunaipa nchi yetu fursa kubwa ya
kujiletea maendeleo, zipo pia changamoto zake.
Hatuna budi kuzitambua na kuzitafutia ufumbuzi ili gesi iweze kunufaisha
ipasavyo nchi yetu na watu wake. Changamoto
zipo nyingi lakini kubwa zipo za namna tatu.
Changamoto ya
kwanza ni ile ya kujenga uwezo wetu wenyewe wa kudhibiti shughuli zinazofanywa
na makampuni ya mafuta ili tuhakikishe kuwa tunapata malipo yanayostahili. Inatulazimu tuwe na wataalamu wetu wazalendo
wa fani za taaluma zihusuzo gesi kama vile uhandisi, kemia, jiofizikia,
uhasibu, ukaguzi na sheria. Tusipojenga
uwezo wetu wenyewe kwenye maeneo hayo kuna hatari ya kudhulumiwa na kupata
hasara. Pengine ipo haja ya kuwa na
chombo maalum kwa ajili hiyo kama tulivyofanya kwa mafanikio kwa upande wa
dhahabu.
Changamoto ya
pili ni ile ya kupata Watanzania wengi wenye ujuzi na taaluma zinazohitajika na
soko la ajira la sekta ya gesi.
Tusipofanya hivyo makampuni yataajiri watu hao kutoka nje na hivyo
kufanya Watanzania kutokunufaika na fursa za ajira zilizopo.
Ndugu Wananchi,
Kwa changamoto
hizi mbili, jawabu lipo kwenye elimu na mafunzo tunayotoa kwa vijana wetu
katika shule, vyuo vya ufundi na vyuo vya elimu ya juu. Kwanza kabisa lazima tuboreshe elimu ya
sayansi na hisabati katika shule zetu za msingi na sekondari. Katika vyuo vya ufundi tutoe mafundi mchundo
wa taaluma zinazohitajika na tasnia ya gesi na mafuta. Hivyo hivyo kwa upande wa vyuo vikuu nako
wafundishe wataalamu wa fani zinazohitajika kama vile utafutaji wa gesi na
mafuta, uendelezaji wa mafuta na gesi, uchumi na biashara ya mafuta na gesi,
uhasibu na ukaguzi wa mafuta na gesi pamoja na sheria za mafuta na gesi na
mikataba ya utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwahakikishia kuwa tayari tumejipanga kutafuta ufumbuzi wa changamoto
hizo. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
kinajiandaa kuanza kutoa mafunzo ya Chemical
and Environmental Lab for Oil and Gas na fani ya Exploration and Production Software Technology katika mwaka huu wa
masomo. Chuo cha Madini Dodoma kitaanza kutoa mafunzo ya diploma ya Petroleum Geoscience kuanzia Septemba
mwaka huu. Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson
Mandela Arusha, na Chuo cha Teknolojia cha Mbeya na kile cha Dar es Salaam pia wameanza kufundisha mitaala hiyo. Aidha,
VETA Makao Makuu na VETA Mtwara nao wanafundisha masomo yahusuyo gesi. Wizara ya Nishati na Madini itawadhamini wanafunzi 50 kutoka Mkoa wa Mtwara
kwenda kupata mafunzo hayo ya gesi asili katika chuo cha VETA Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Wizara ya Nishati
na Madini pia inatekeleza mpango mkakati wa kuwapata wataalamu wa sekta hiyo kati
ya 40-50 kati ya sasa na mwaka 2016. Taaluma zinazotiliwa mkazo ni Petroleum Geoscience, Petroleum Geophysics,
Petroleum Geochemistry, Petroleum Engineering, Petroleum Modeling, Oil and Gas
economics, Oil and Gas Accounting and Auditing na Oil and gas Legal Regimes and
Contract Negotiations. Kwa upande
wake, Serikali itatoa upendeleo maalum kwa kulipia gharama zote za mafunzo ili
tuweze kuwapata wataalamu hawa mapema iwezekanavyo. Nawaomba vijana wetu wachangamkie
fursa hizi za masomo na watakapohitimu mafunzo wawe tayari kuitumikia nchi yetu
kwa bidii.
Kujenga
Uwezo Wetu wa Kutumia Mapato ya Gesi
Ndugu Wananchi,
Changamoto
nyingine kubwa sana ni ile ya kuhakikisha kuwa mapato yatokanayo na gesi
yanatumika vizuri na kwa manufaa ya taifa na watu wake. Lazima tuanze sasa kufikiria na kujipanga kwa
ajili hiyo. Si vyema tukangojea mpaka
hapo mapato yatakapoanza kupatikana ndiyo tufikirie na kutengeneza mfumo mzuri
wa kusimamia na kutumia mapato yatokanayo na gesi. Tutakuwa tumechelewa, watu laghai na waovu
watakuwa wameanza kunufaika hivyo watakuwa wagumu kutengeneza mfumo utakaowanyima
fursa ya kuliibia taifa.
Jambo hili ni
muhimu sana kufanya kwani ipo mifano hai ya nchi zenye rasilimali nyingi za
mafuta na gesi lakini nchi na wananchi wake hawanufaiki sawia. Mauzo yanafanyika na fedha nyingi kupatikana lakini
manufaa kwa nchi na watu wake ni madogo
au hayapo kabisa. Wanaonufaika ni
viongozi na baadhi ya maofisa wa umma wanaohusika na usimamizi wa shughuli zihusuzo
rasilimali hizo. Na, hata sisi tunaweza
kujikuta katika hali hiyo kama tusipojipanga vizuri sasa ambayo badala ya
rasilimali kuwa baraka zinageuka kuwa balaa au hata laana.
Ndugu Wananchi;
Zipo nchi
duniani ambazo zina usimamizi mzuri wa mapato ya rasilimali za mafuta na gesi
na kuleta baraka na neema kwa taifa na watu wake. Nchi hizo zimeweza kuhifadhi na kutumia
vizuri mapato yake kukuza uchumi wa nchi kwa jumla na kuboresha upatikanaji wa
huduma za kiuchumi na kijamii kwa watu. Matokeo
yake ni watu wa nchi hizo kuishi maisha yaliyo bora kuliko walivyokuwa kabla ya
kupatikana kwa rasilimali hizo. Lakini,
hii imewezekana kutokana na usimamizi mzuri na matumizi mazuri ya mapato
yatokanayo na mafuta na gesi.
Tumeamua kujifunza kutoka nchi za wenzetu waliofanikiwa
ili na sisi tunufaike. Na sisi
tunajiandaa kutengemeza Sera ya Gesi Asili na kurekebisha Sheria ya Utafutaji
na Uzalishaji wa Mafuta na Sheria ya Menejimenti ya Mapato ya Serikali
yatokanayo na gesi zitakazotoa majibu hayo na kuliwezesha taifa kuwa na mfumo
mzuri wa usimamizi wa utafutaji na uchimbaji wa gesi asili pamoja na usimamizi na
matumizi mazuri ya mapato yatokanayo na gesi hiyo. Wapo wenzetu kwa mfano, wanacho kitu
kinachoitwa Sovereign Funds ambapo mapato yote huhifadhiwa na baadae hutolewa
kwa utaratibu maalum. Tunataka
tujifunze kutoka kwao ili na sisi tutengeneze chombo chetu cha namna hiyo ili
tunufaike.
Ndugu Wananchi;
Mambo hayo
tumeshaanza kuyafanyia kazi. Katika
mazungumzo yangu na baadhi ya wakuu wa nchi rafiki na mashirika ya maendeleo ya
kimataifa, nimewasilisha maombi ya kusaidiwa na kushirikiana kwa mambo
mawili. Kwanza kwa kuwawezesha
Watanzania kupata mafunzo ya haraka kwa wataalamu watakaosaidia kusimamia
shughuli za utafutaji, uendelezaji na biashara ya gesi asili nchini. Pili, watusaidie kupata watu wenye ujuzi na
uzoefu ili watushauri kuhusu namna ya kutengeneza mifumo bora ya kusimamia na
kutumia mapato ya gesi kwa mujibu wa mifano ya wenzetu waliofanikiwa. Nafurahi kwamba maombi yetu yamepokelewa vizuri
na nchi zote na mashirika yote ya kimataifa tuliozungumza nao. Baada ya muda si mrefu kazi itaanza.
Mgomo wa
Walimu
Ndugu Wananchi;
Jambo la tatu na la mwisho ni mgomo wa walimu. Pengine ni mapema kusema kwa vile
kesho Mahakama itaamua kuhusu shauri hilo.
Lakini napenda kuwahakikishia walimu kuwa tunawajali, tunawathamini na
kutambua mchango wao muhimu kwa taifa letu.
Wakati wote tumekuwa tunashughulikia madai ya haki zao na malimbikizo
mbalimbali. Madai ya safari hii ni
makubwa mno, yametuzidi kimo. Athari za
kuyatimiza yalivyo yataifanya bajeti ya Serikali kutumia asilimia 75 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali na
kubakiza asilimia 25 kwa kuendeshea
Serikali na kutimiza majukumu ya maendeleo kwa wananchi. Haitakuwa sawa. Ndiyo maana tumeshindwa kuelewana walipokataa
rai hiyo na wao kusisitiza kugoma.
Wakati tunaendelea kusubiri uamuzi wa Mahakama, nina maombi mawili kwa
walimu: Moja, wasiwalazimishe walimu
wasiotaka kugoma wafanye hivyo, wawaache waendelee na kazi. Pili, wasitumie watoto isivyostahili kujenga
hoja zao. Nawasihi warudi kwenye meza ya
mazungumzo.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu naomba nitumie fursa hii kuwatakia
Waislamu wote nchini kheri na baraka tele kwa swaumu ya mwezi mtukufu wa
Ramadhan. Wakati wote, mjiombee wenyewe kwa Mwenyezi Mungu awajaalie toba na malipo
mema katika mfungo huu. Mkumbuke pia
kuiombea nchi yetu amani, upendo na mafanikio mema.
Baada ya maneno hayo, naomba sasa
niishie hapo. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza. Sasa nipo tayari kujibu maswali ya Wahariri kama
yapo. Ndugu Wahariri mliopo hapa, karibuni.
No comments:
Post a Comment